Subscribe:

Ads 468x60px

Saturday, October 5, 2013

Yanga wamleta Mfaransa wa Simba Dar

Kocha Mfaransa, Patrick Liewig aliyewahi kuinoa timu ya Simba kabla ya kutimuliwa

KOCHA Mfaransa, Patrick Liewig anatamani Yanga iifunge Simba ili awe shuhuda wakati viongozi wa Msimbazi wanapomtimua kazi kocha wao, Abdallah Kibadeni.
Kocha huyo ametoa kali zaidi baada ya kuwatuhumu viongozi wa Simba kuwa walikuwa wanampangia kikosi uwanjani.
Liewig amesema Oktoba 20 atakuwa kwenye jukwaa la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kushuhudia kama Simba itamtimua kocha wake wa sasa iwapo watafungwa na mahasimu wao Yanga katika Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo aliliambia Mwanaspoti kutoka Paris, Ufaransa kuwa sababu kubwa iliyomfanya afutwe kazi na Simba ni kichapo kutoka kwa Yanga, hivyo atahakikisha anahudhuria mechi hiyo ili kuona kama kocha mpya wa vinara hao wa Ligi Kuu msimu huu, Abdallah Kibadeni atafukuzwa kazi iwapo atafungwa na watani wao wa jadi katika mechi hiyo ya kukata na shoka.
Liewig alisema atawasili Dar es Salaam Oktoba 18 mwaka huu kushuhudia mchezo huo, kisha atawafuata viongozi wa Simba ili wamlipe fedha anazowadai Dola za Marekani 16,000 (Sh26 milioni).
“Nitaenda kuona wakimfukuza kocha iwapo watafungwa na Yanga kwani ndio tabia ya viongozi wa klabu hiyo kufanya hivyo. Najua kocha atapangiwa kikosi na viongozi au mashabiki,” alisema Liewig.
Liewig anasema kama kuna kitu kiliwahi kumkera katika maisha yake yote ya ukocha, basi ni kauli iliyowahi kutolewa na kiongozi wa Simba kwamba anatimuliwa klabuni hapo kwa sababu alifungwa na Yanga kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu msimu uliopita huku wakiwa wamempangia kikosi.
“Kinachoigharimu Simba ni kutokuwa na viongozi wanaojua mpira, wamezidi siasa. Kibaya zaidi ni ile tabia yao ya kumpangia kocha kikosi wakisema kuwa hicho ndicho kikosi kinachoweza kucheza na timu fulani hususani Yanga,” alisema.
“Mimi kwenye maisha yangu yote mpaka sasa nina miaka 62 sijawahi kuona kiongozi wa soka akimpangia kocha kikosi cha kucheza na timu fulani.”
Liewig aliongeza: “Nashughulikia hati yangu ya kusafiri ili nije kudai changu na kutazama mechi yao dhidi ya Yanga. Sitahitaji usumbufu na viongozi wa Simba kuhusiana na malipo ya usafiri, ninachohitaji ni kilicho changu pekee.”
Katika mechi ya kumalizika msimu uliopita, Yanga iliichapa Simba mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuanzia hapo Liewig, ambaye alikuwa kocha wa klabu hiyo ya Msimbazi ikawa ndio mwisho wa ajira yake.

0 comments: