Shindano la mbio za Kilimanjaro Marathon 2014 liko mbioni kuanza Machi 2014, huku waandaaji wa shindano hilo wakiwa wameongeza zawadi zaidi ya Sh milioni 40 kwa washindi wa shindano hilo na kuzifanya mbio hii kuwa kati ya mbio kubwa zaidi barani Afrika..
Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers,ambao pia ni waandaaji wa shindano hilo, John Addison alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa mbali na zawadi hiyo ya fedha, washindi pia watajishindia zawadi nyingine nono kutoka kwa wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager kwa kushirikiana na wadhamini shirikishi.
Addison alisema washindi wa mbio ndefu za marathoni za kilometa 42, watajishindia Sh milioni 20, na zawadi ya fedha taslimu Sh milioni 10 kwa washindi wa nusu marathon huku washindi wa mbio za walemavu maarufu kama GAPCO 10km Marathon wakijishindia Sh milioni sita.
Washiriki wote watakaomaliza mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run watajishindia zawadi mbalimbali. Alisema mbio za mwaka huu zimesheheni motisha mbalimbali za kuvutia ili kuongeza idadi ya washiriki.
Washindi wa kwanza katika marathoni wanawake kwa wanaume watajinyakulia Sh milioni 4 kila mmoja, Sh milioni 2 kwa washindi wa pili na Sh milioni 1 kwa washindi wa tatu.
Washindi wa kwanza katika nusu marathoni wanawake kwa wanaume watapewa Sh milioni mbili kila mmoja, Sh milioni 1 kwa washindi wa pili na Sh 500,000 kwa washindi wa tatu.
Addison alisema medali na fulana zitatolewa kwa wanariadha 500 wa kwanza kumaliza mbio za kilometa 42, wanariadha 2,200 wa kwanza kumaliza mbio za nusu marathon na wanariadha 80 wa kwanza kumaliza mbio za walemavu.
“Washiriki 3,000 wa kwanza kumaliza mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run watapewa fulana baada ya kumaliza mbio na watapata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali za kuvutia kupitia droo,” alisema mkurugenzi huyo.
Ili kuwapa hamasa wanariadha wa Tanzania kufanya vizuri katika mbio hizo, Kilimanjaro Premium Lager imetenga Sh milioni mbili kama bonasi kwa wanariadha Watanzania watakaovunja rekodi katika mbio hizi.
Mbio hizo zinaratibiwa na kwa kushirikiana na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, Kibo Palace Hotel, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.
0 comments:
Post a Comment