Viongozi mbali mbali pamoja na raia wa Afrika Kusini wanaendelea kutoa heshma za mwisho kwenye mwili wa aliyekuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini Marehemu Nelson Mandela ambao umelazwa kwenye ikulu ya Afrika Kusini mji Mkuu wa Pretoria, ambapo utalala hapo kwa siku tatu.
Mwili ulichukuliwa katika msafara kutoka chumba cha maiti cha hosptali hadi kwenye jengo la Muungano.
Msafara wenye jeneza la Marehemu uliondoka mjini katika Hosptali ya jeshi muda mfupi siku ya jumatano. Jeneza lilibebwa kwenye gari maalum na kufunikwa bendera ya Afrika Kusini.
Wananchi walijipanga kando kando ya barabara lilipopitishwa jeneza kama ishara ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu.
Wanajeshi waliobeba jeneza hilo walisonga hatua kwa hatua hadi katika Majengo ya Muungano eneo alikoapishwa kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika kusini 1994.
Wanachi, wakuu wa nchi walioalikwa na wageni wengine wa kimataifa watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho kwenye mwili wa marehemu aliyefariki alhamisi akiwa na umri wa miaka 95.
Wageni hata hivyo hawaruhusiwa kupiga picha.
Leo jioni wasanii mbali mbali wa Afrika Kusini watashiriki katika tamasha maalum la kumuenzi Mandela na ambalo wananchji wataruhusiwa kuhudhuria bila malipo.
Marehemu Mandela atazikwa nyumbani kwake katika kijiji Qunu katika jimbo la Cape Mashariki siku ya jumapili.
0 comments:
Post a Comment